TANZANIA KUSHEREHEKEA MIAKA 100 YA USKAUTI TAREHE 22-29 JULAI 2017
Mwaka huu skauti wote wa Tanzania tunatarajia kufanya sherehe kubwa ya kitaifa itakayowahusisha wageni wa kimataifa. Sherehe hii itakuwa ni Jubilei ya miaka 100 tangu mafunzo na elimu ya skauti iingie Tanzania.
Tunafundishwa na historia kuwa Uskauti ulianza rasmi kule Magila Muheza Tanga mwaka 1907. Wakati huohuo uskauti uliingia kwenye mikoa ya Kagera, Dar es Salaam na maeneo ya kusini mwa nchi. Wahusika wa uingizaji wa uskauti nchini walikuwa wamisionari wa Kikristo na Waasia kwa mkoa wa Dar es Salaam.
Pamoja na kuwa uskauti uliingia kwa milango hiyo mingi, Magila inatazamwa kuwa ndio mlango muhimu zaidi kwani hata Mwanzilishi wa skauti duniani, Lord Baden Powell alipatambua hapo na akapatembelea mnamo mwaka 1935.
Maadhimisho ya Jubilei yatafanyika Mkoa wa Dodoma kwenye eneo la viwanja vya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Tarehe ya kuwasili ni 21/07/2017. Kambi litaanza tarehe 22/07/2017. Kambi litafungwa tarehe 29/07/2017. Ada ya Ushiriki ni TZS 65,000/= tu. Washiriki watajitegemea usafiri wa kwenda na kurudi Dodoma.
Serikali imeonesha utayari wa kuhamasisha mafanikio ya sherehe hii kwa kuwaagiza viongozi wa mikoa, wilaya na Halmashauri kuhakikisha vijana wasiopungua 20 wanawezeshwa kushiriki kwenye sherehe hizo.
Inashauriwa kulipia ada ya kambi kwa njia ya benki kupitia akaunti ifuatayo: Tanzania Scouts Association - Centenary and ASD 2017. Account Number: 0150260555200.
Kamati ya maandalizi ya sherehe hizi itapokea kwa shukrani michango ya hali mali kutoka kwa mtu yeyote ndani na nje ya Tanzania. Michango itumwe kwenye akaunti tajwa.
Inafaa washiriki wote tufanye maandalizi ya dhati kuelekea kambi hiyo. Baadhi ya mambo tunayotakiwa kuwa tumeyafanyia kazi au kuwa tunayafanyia kazi kwa sasa ni haya:
- Matayarisho ya eneo la shughuli kuahakikisha huduma za maji, vyoo, umeme, matibabu, ulinzi, usafiri na dharura vipo.
- Kuhakikisha kuwa timu ya skauti wanaojitolea kuleta mafanikio ya shughuli hasa katika kuwaelekeza wageni na kusogeza huduma imetajwa na inapewa mafunzo.
- Kuhakikisha kuwa huduma za chakula na vinywaji imeandaliwa ipasavyo.
- Kuhakikisha vitu vitakavyokuwa kumbukumbu kwa washiriki, mathalani skafu, kofia, fulana au mifuko vinaandaliwa.
- Kuhakikisha matangazo ya shughuli yanfanyika kupitia vipeperushi, vyombo vya habari na makongamano ya maandalizi.
- Kuhakikisha kuwa huduma za malazi ya washiriki kama vile mahema, mabweni na hoteli zipo na mipango imethibitishwa.
- Kutayarisha bendera za mataifa yote yatakayoshiriki.
- Kutoa mialiko kwa wadau wote hasa marafiki wa skauti, wastaafu, na wadau wanaoshughulikia maswala ya vijana sambamba na skauti.
- Kuongeza mawasiliano kati ya kamati ya kitaifa na kamati ya mkoa wa Dodoma na skauti mikoa yote.
- Kuteua timu ya uendeshaji wa kambi mapema iwezekanavyo ili shughuli ya kuteua, kupanga, kuandaa shughuli vitendo za maadhimisho zifanyike mapema kwa ufanisi.
- Kuandaa tuzo maalumu za miaka 100 na kuwatunukia baadhi ya watu waliotoa mchango wa pekee kwenye Chama cha Skauti Tanzania, mathalani, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Brigedia Hashimu Mbita, Dr. Leader Sterlings, Mzee Isdori Ngunga, Raisi Mstaafu Ali Hassan Mwinyi, na wengine wanaostahili.
- Kuandaa vifaa vya kufanyia mafunzo na maonesho ya kiskauti.
- Kuandaa vifaa binafsi vya kambi la kiskauti.
Orodha hii si kamili. Ninaamini wasomaji wataongeza vigezo vingine vya kuzingatiwa (checklist) kuelekea sherehe hizi muhimu kwa chama hiki cha kielimu nchini Tanzania.
Maandalizi ya wakati huepusha mfadhaiko, msongo na msongamano. Tuanze kwenda Dodoma kwe sherehe kwanza kifikra na hatimaye kikamilifu.